Kasisi aliyefariki baada ya kuangukiwa na msalaba alikuwa akiongoza misa mubashara Ecuador

Chanzo cha picha, Facebook/perpetuosocorrogye
Kuanguka ghafla kwa msalaba na kumuangukia kichwani kasisi aliyefariki kutokana na majeraha aliyoyapata wakati akiendesha ibada ya Misa,imeizamisha jamii ya Wakatoliki mjini Guayaquil, Ecuador, katika maombolezo.
Tukio hilo lilitokea katika Kanisa la Our Lady of Perpetual Help, katikati mwa mji wa Guayaquil nchini Ecuador, siku ya Jumamosi wakati kasisi Patricio Alfredo Sánchez Molinari alipokuwa akiongoza ibada ya kawaida ya Misa.
Sánchez Molinari, mwenye umri wa miaka 53, alikuwa kwenye madhabahu akiongoza ibada ya misa wakati msalaba mkubwa wa mbao ulipolegea ghafla kutoka mahali ulipokuwa umetundikwa ukutani na kumuangukia moja kwa moja.
Kasisi huyo alianguka chini mara moja, huku waumini waliokuwa wamehudhuria ibada hiyo pamoja na wengine waliokuwa wakifuatilia matangazo ya moja kwa moja kupitia mitandao ya kijamii wakishuhudia tukio hilo kwa mshangao mkubwa.
Jimbo Kuu la Kanisa Katoliki la Guayaquil lilithibitisha kifo cha Sánchez Molinari Jumamosi usiku.
Katika taarifa yake, jimbo hilo lilisema: "Tunashukuru kwa ujumbe wote wa rambirambi kutoka sehemu mbalimbali za dunia na, hasa, kwa maombi yenu kwa ajili ya roho ya Padri Patricio Sánchez, ili ipumzike kwa amani ya milele."
Kadinali Luis Cabrera, Askofu Mkuu wa Guayaquil, aliongoza ibada ya Misa siku ya Jumapili katika kanisa hilohilo la Our Lady of Perpetual Help, ambako ajali hiyo ilitokea, kwa ajili ya kumuenzi kasisi huyo.
Hakukuwa na taarifa kuhusu kilichosababisha msalaba huo kulegea na kuanguka.

Chanzo cha picha, Redes
"Iteni ambulensi! Padri, Padri!"
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Muda mfupi kabla ya ajali hiyo, kasisi huyo alikuwa ametoa mahubiri yake, ambapo aliwaomba waumini kutafakari muda wanaoutumia kumtumikia Mungu katika maisha yao ya kila siku na kujiuliza iwapo wanatumia muda huo mwingi kama ule wanaotumia katika mambo ya muda mfupi, kama vile simu za mkononi au kutazama vipindi vya televisheni.
"Ndugu zangu wapendwa, siku moja sisi sote tuliopo hapa tutakufa," alisema katika mahubiri yake.
"Na wakati mwingine, muda tunaotumia katika mambo yasiyo na maana sana haulingani na ule tunaotumia kuwa pamoja na Mungu. Muda bora tunaoutumia kwa ajili ya Mungu, ndugu na dada zetu, waume na wake zetu, watoto wetu na familia zetu huo ndio muda unaotumika vizuri zaidi," aliongezea.
Baada ya kumaliza mahubiri yake, kasisi huyo alirejea kwenye madhabahu na kuongoza sala za ibada ya Misa.
Hata hivyo, ajali hiyo ilitokea wakati huo, dakika mbili tu baada ya kumaliza mahubiri yake.
"Padri, Padri!" alisema mwanamke mmoja aliyekuwa akimsaidia kasisi huyo karibu na madhabahu. "Iteni ambulensi! Padri, Padri!"
Vyombo vya habari vya eneo hilo vilionesha picha siku ya Jumatatu, ambapo shughuli ya kurejesha sanamu ya Yesu msalabani mahali pake pa awali ndani ya kanisa hilo ilikuwa ikiendelea.

Chanzo cha picha, Arquidiócesis de Guayaquil
Imetafsiriwa na Beldeen Waliaula na kuhaririwa na Ambia Hirsi
































